Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Kundi la wanazuoni wa Bahrain limetoa taarifa likiitaka serikali ya nchi hiyo kuwaachilia mara moja na bila masharti wanazuoni wa dini waliokamatwa, kufuta mashtaka yote wanayodai kuwa ni ya kubuni, na kusitisha vitendo vya mateso, udhalilishaji na vikwazo vinavyowekwa dhidi yao.
Katika taarifa hiyo, wanazuoni hao wameieleza serikali ya Bahrain kuwa inawajibika kikamilifu kwa usalama na afya ya wanazuoni hao wakati wote wa kipindi chao cha kizuizini, wakionya kuwa wataiwajibisha kwa madhara yoyote ya kimwili au kisaikolojia yatakayowapata.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa wimbi la kukamatwa kwa wanazuoni wa Kishia ni sehemu ya juhudi zinazolenga kudhoofisha mamlaka ya kidini na kuondoa sauti ya elimu, fatwa na mwongozo wa dini katika jamii ya Bahrain.
Aidha, wanazuoni hao wamedai kupokea taarifa zinazoonyesha kuwa baadhi ya waliokamatwa wamekumbwa na mateso ya kimwili na kisaikolojia, pamoja na kushinikizwa kusaini maungamo na nyaraka mbalimbali. Pia, wanadaiwa kutishwa kwa kunyimwa uraia, haki zao za kisheria na kutukanwa kutokana na imani na madhehebu yao.
Wanazuoni wa Bahrain wamesisitiza kuwa wanazuoni ni warithi wa Mitume, walinzi wa Sharia na wabebaji wa dini, hivyo kuwashambulia ni kushambulia utambulisho na misingi ya Umma wa Kiislamu.
Mwishoni mwa taarifa yao, wamelaani hatua hizo kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa kuabudu, uhuru wa kuamini na heshima ya binadamu, wakisisitiza kuwa vitisho, kukamatwa na ukandamizaji haviwezi kuzima nuru ya elimu, fiqhi na mshikamano wa waumini katika kushikamana na dini yao.
16 Julai 2026 - 12:43
Msimbo wa Habari: 1840983
Wanazuoni wa Bahrain wametoa wito wa kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa wanazuoni wa dini waliokamatwa, wakiiwajibisha serikali ya Bahrain kwa madhara yoyote ya kimwili au kisaikolojia yatakayowapata wakiwa mahabusu.
Maoni yako